Na Lydia Churi- Mahakama, Arusha Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imefanikiwa kusikiliza na kumaliza kwa zaidi ya asilimia 90 ya mashauri yaliyofunguliwa katika kipindi cha mwezi Januari hadi Agosti mwaka huu. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kanda ya Arusha Mhe. Angelo Rumisha, jumla ya mashauri 737 kati ya 805 yaliyosajiliwa kuanzia mwezi Januari hadi Agosti 2017, yamemalizika. Alisema haya ni mafanikio ya kuridhisha kwa Mahakama Kuu kanda ya Arusha ambapo kila Mhe. Jaji amesikiliza na kumaliza wastani wa mashauri 245. Hivi sasa, Mahakama Kuu kanda ya Arusha ina jumla ya majaji watatu. Katika kuhakikisha inaondokana na mlundikano wa mashauri kwenye Mahakama mbalimbali nchini, Mahakama ya Tanzania ilipanga idadi ya mashauri yatakayosikilizwa na Majaji na Mahakimu. Kwa mujibu wa mpango huo, kila Jaji anatakiwa kumaliza mashauri yasiyopungua 220 kwa mwaka na hakimu Mashauri 250. Akifafanua takwimu za mashauri, Naibu Msajili alisema hadi kufikia Agosti 31, mwaka huu, Mahakama hiyo imebakiwa na mashauri 809 ambapo kati ya mashauri hayo, 788 yana umri wa kati ya miaka 1-2, mashauri 17 yana umri kati ya miaka 3-5, mashauri 2 yana umri kati ya miaka 5-10 na mashauri mengine 2 yana umri wa zaidi ya miaka 10. Alisema mashauri yote yenye miaka 10 na zaidi ni yale yaliyorudishwa kutoka Mahakama ya Rufani baada ya kikao cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kilichofanyika April mwaka huu. Akizungumzia Mahakama za Hakimu Mkazi na za Wilaya kwa Mikoa ya Arusha na Manyara, Mhe. Rumisha alisema jumla ya mashauri 223 yana umri zaidi ya miezi 12, kati ya mashauri hayo, ni mashauri mawili tu ndiyo ambayo Mahakama zina mamlaka nayo ikiwa ni sawa na asilimia 1.3 ya mashauri yote yenye umri zaidi ya miezi 12 hivyo mashauri mengi ya mlundikano ni yale ambayo Mahakama hazina mamlaka nayo. | |
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kanda ya Arusha Mhe. Angelo Rumisha |
0 Comments